#mdstickybar { background-color:#ECEEF5; padding-top:10px; width:300px!important; padding-bottom:15px; color:#474747; }
Latest Updates

Serikali yawakana walimu, Maneno ya Maaskofu kwa SLAA,MAGUFULI,Rufaa za wagombea..#StoriKubwa







NIPASHE

Jeshi la Polisi Mkoani Kilimanjaro limemshikilia na kumhoji kwa zaidi ya saa tano mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Vijijini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa chama hicho, Anthony Komu , kwa madai ya kumtisha kwa bastola Katibu wa chama hicho mkoani hapa, Basil Lema.

Hata hivyo, baada ya kuhojiwa jeshi hilo lilimwachia huru Komu na kisha kulifuta jalada la uchunguzi lililofunguliwa dhidi yake baada ya mlalamikaji (Lema) kuomba shauri hilo limalizwe katika meza ya usuluhishi ndani ya Chadema.

Komu alisema alishikiliwa na kuhojiwa kuanzia saa 5:00 asubuhi na kuachiwa saa 10:00 jioni.

“Niliwaeleza kwamba sijawahi kumiliki silaha na sina mpango wa kuimiliki wakaridhika na maelezo yangu na wakakubali mzozo uliotufikisha hapo tukaumalize nje ya vyombo vya sheria,” alisema.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoani Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani, alithibitisha kwamba mgombea huyo wa ubunge Jimbo la Moshi Vijijini kupitia Chadema alikuwa alitumiwa ujumbe wa kuitwa polisi kwa ajili ya kuhojiwa kuhusiana na tuhuma hiyo.

Agosti 18, mwaka huu wakati wa marudio ya uchaguzi wa kura ya maoni za Chadema katika jimbo hilo, Komu akiwa katika eneo la Kibosho, Moshi Vijijini alidaiwa kumtisha kwa bastola katibu huyo wa mkoa alipomfuata akitaka kujua taratibu zilizotumika kuhamisha mkutano wa uchaguzi huo ambao ulipangwa kufanyika katika eneo la Garden, kata ya Kiboroloni, Manispaa ya Moshi.

Naye Lema akizungumzia suala hilo alisema: “Ni kweli tumemalizana na bosi wangu (Komu) baada ya kuafikiana wenyewe na kuomba polisi ikubali mambo haya yamalizwe nje ya vyombo vya kisheria kutokana na maslahi mapana ya Chadema.”

NIPASHE

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema asilimia kubwa ya maandalizi ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu yamekamilika, huku karatasi za kupigia kura zikitokea Afrika Kusini.

Aidha, tume hiyo imesema gharama za awali kwa ajili ya ununuzi wa vifaa mbalimbali kama vile wino, fulana, kofia, karatasi za kura, vibanda vya kupigia kura na vifaa vya kufungashia katika uchaguzi huo hadi sasa zimefikia Sh. bilioni 31.25.

Imesema dola za Marekani 6, 145, 882.92 sawa na Sh. bilioni 13.1 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya ununuzi karatasi hizo za kura. Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Manunuzi na Menejimenti ya Lojistiki wa Nec, Eliud Njaila, wakati akizungumza Dar es Salaam jana.

Alisema karatasi hizo zinatarajia kuanza kuwasili nchini Septemba 29 hadi Oktoba 15, mwaka huu.

Alisema gharama za vifaa hivyo ni tofauti na zile zilizotumiwa na tume hiyo kwa ajili ya kununulia mashine 8,000 za Biometric Voters Registration (BVR) na shughuli nzima ya uandikishaji kwenye Daftari la Wapigakura nchi nzima, ambazo kwa mujibu wa Nec ni Sh. bilioni 133.

Tume hiyo pia ilisema Sh. bilioni 85 zilitumika kulipa posho waandikishaji, wataalamu wa mashine hizo, kutengeneza kadi, karatasi, wino na vifaa muhimu wakati wa uandikishji kwenye daftari hilo nchini kote.

Alitaja kampuni iliyoshinda zabuni ya wazi ya kutengeneza karatasi hizo kuwa ni Uniprint ya nchini Afrika Kusini ambayo alisema ina uzoefu mkubwa katika kazi hiyo kwani ndiyo iliyoshinda zabuni ya kutengeneza vifaa hivyo katika uchaguzi mkuu nchini humo wa Tanzania wa mwaka 2005.

NIPASHE

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imepokea rufaa 54 za madiwani kupinga maamuzi ya wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo mbalimbali nchini.
Taarifa ya Nec iliyotolewa jana, ilieleza kupokea pia jumla ya rufaa 198 za madiwani kutoka Halmashauri mbalimbali.
“Tume imeanzakupitia vielelezo vilivyowasilishwa na wagombea (warufani) na wasimamizi wa uchaguzi kutoka majimboni. Imeanza kuzitolewa maamuzi rufaa za Wabunge,” taarifa hiyo ilieleza na kuongeza:
“Leo (juzi) zimejadiliwa na kuamuliwa rufaa 38. Zilizobaki mawasiliano yanaendelea kati ya tume na wasimamizi wa uchaguzi ili kupata vielelezo vinavyohusika kuisaidia Tume kufikia maamuzi ya kisheria na haki kwa wagombea na vyama vyote vinavyoshiriki katika uchaguzi.”
Iliongeza kuwa wagombea waliokuwa wamewekewa pingamizi na kuenguliwa na wasimamizi wa uchaguzi ni 16 na Tume imerudisha wagombea 13 kati ya hao, waliobaki ni 3 ambao Tume imeridhia maamuzi ya wasimamizi wa uchaguzi.
“Hii ni kutokana na vielelezo vilivyowasilishwa kutoonesha makosa ya kisheria au kiufundi,” iliongeza taarifa hiyo.

NIPASHE

Sakata la madeni ya walimu limezidi kuchukua sura mpya baada ya serikali kusema haidaiwi na kwamba imebaini kuwapo kwa majina hewa ya walimu zaidi 4,000 yaliyowasilishwa kwa ajili ya malipo.

Imesema imegundua hivyo baada ya kufanya uhakiki wa deni la Sh. bilioni 19.6 lililowasilishwa na walimu baada ya kuwalipa madai yao kwa mara ya mwisho mwaka 2013.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile, baada ya kuhakiki madeni hayo mwaka jana, serikali imegundua deni halisi inalodaiwa na walimu ni Sh bilioni 5.6 tu.

Alisema endapo serikali isingefanya uhakiki wa deni hilo na kulilipa ingeingia hasara ya Sh. bilioni 14.

Alisema katika uhakiki huo, wizara hiyo imebaini kulikuwa na deni hewa kubwa la mwalimu mmoja wa Halmashauri ya Tunduru Mkoani Lindi Sh. milioni 500 na kwamba baada ya kuhakiki imegundua deni lake halali ni Sh. 500,000 tu.

Dk. Likwelile alisema kwa madeni ya mwaka jana, serikali imelipa walimu Sh. bilioni 5.6 baada ya kufanya uhakiki.

“Katika uhakiki tumebaini kuwapo udanganyifu wa fedha kwa walimu kujiongezea huku wengine wakidai deni la aina moja mara nne,” alisema.

Dk. Likwelile alitaja sababu za serikali kukataa kulipa baadhi ya madai ya walimu yaliyowasilishwa ni pamoja na kukosa vibali au vielelezo, madai mengine kuwa yameshalipwa, mishahara iliyowasilishwa kama madai yasiyo ya mishahara, baadhi ya walimu kutotambuliwa na halmashauri, baadhi ya walimu kutokuwa na madai katika majalada na makosa ya ukokotoaji na uandishi.